Dar es Salaam na Iringa. Waziri wa Fedha na
Mbunge wa Kalenga (CCM), Iringa, William Mgimwa amefariki dunia jana
katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini alikokuwa
akitibiwa.
Habari zilizopatikana jana kutoka Ubalozi wa
Tanzania nchini Afrika Kusini kupitia kwa Msemaji wake, Habib Awesi
zilisema Waziri Mgimwa amefariki dunia mchana... “Ni kweli amefariki leo
mchana tumepeleka taarifa Ikulu, Dar es Salaam.”
Baadaye jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kusema Waziri
Mgimwa alifariki dunia saa 5:20 kwa saa za Afrika Kusini (saa 6:20).
“Kinachofanyika kwa sasa ni maandalizi ya
kuurudisha nyumbani mwili wa marehemu na hilo linafanywa na Serikali kwa
kushirikiana na familia yake. Taarifa zaidi zitatolewa baadaye kadiri
zitakavyopatikana,” alisema Balozi Sefue.
Akizungumzia msiba huo, Naibu Spika wa Bunge, Job
Ndugai alisema: “Bunge limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Dk
Mgimwa, alikuwa ni mtu mwaminifu katika kazi zake na alishirikiana
kikamilifu na wabunge katika kutekeleza kazi za Serikali. Taifa
limepoteza mtu makini aliyefanya kazi katika sekta ambayo aliisomea,
jambo ambalo lilimfanya awe na ufahamu mzuri wa mambo katika wizara
(Fedha),” alisema Ndugai.
Kikwete atuma rambirambi
Jana jioni Rais Jakaya Kikwete alitoa taarifa akielezea kushtushwa na kifo cha Waziri Mgimwa.
“Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za
kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa,” ilisema taarifa yake
kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu.
Alisema taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika
kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa
ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na
mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.
Katika salamu zake kupitia kwa Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda na kwa familia ya marehemu Mgimwa, Rais Kikwete alisema:
“Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia
taarifa za kifo cha Mgimwa.
“Binafsi nilimtembelea mara mbili hospitali
alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika.
Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa
yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.
“Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote
tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu... Natoa
pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana familia wote kwa
kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo
mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni
majonzi yangu,” alisema Rais Kikwete.
Jimboni
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa Vijijini, Steven Muhapa alisema jana kuwa wamepokea kwa mshituko kifo cha mbunge wao.
Muhapa alisema halmashauri yake imepata pigo la
mwaka, kwani walikuwa na mipango mingi ya kutekeleza chini marehemu
Mgimwa lakini sasa imeyeyuka... “Alisaidia sana kutuletelea wafadhili
kutekeleza ahadi mbalimbali alizoahidi... ni mapenzi ya Mungu.”
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa
alisema Mkoa wa Iringa umepoteza mtu muhimu, mahiri na mchapakazi...
“Pamoja na kwamba alikuwa CCM, hakubagua mtu. Niliwahi kumpa ushauri
mara kadhaa akauchukua ushauri wangu na kuufanyia kazi.”
Mwenyekiti PAC
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC), Zitto Kabwe amemwelezea marehemu kwamba alikuwa ni
mtu mnyenyekevu na hakuwa na ubaguzi katika kutekeleza wajibu wake akiwa
kiongozi wa Serikali.
“Kwa kipindi kifupi nilichofanya naye kazi kwa
karibu, kwanza kwenye Kamati ya Fedha, nikiwa mkaribishwa kama Waziri wa
Fedha kivuli, kisha kwenye kamati ndogo niliyounda kuhusu miradi ya
umeme ya Mchuchuma, Liganga na Ngaka na baadaye akiwa Waziri wa Fedha,
jambo la msingi nililoliona kwake ni unyenyekevu na heshima kubwa
aliyonayo kwa watu wengine.
“Hakusita kuomba ushauri licha ya kuwa na tofauti
za kivyama na kwa kweli ni Waziri wa Fedha niliyeelewana naye zaidi
kuliko wengine wote waliopita nikiwa ama Waziri Kivuli au Mwenyekiti wa
Kamati za Hesabu.”
|
Thursday, January 2, 2014
WAZIRI WA FEDHA DKT WILLIAM MGIMWA AFARIKI DUNIA
Labels:
Habari
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment